clock

,,,,,

Wednesday, October 10, 2012

Wanafunzi wazua rabsha Nigeria.

Chuo kimoja kikuu kimefungwa nchini Nigeria baada ya ghasia kuzuka kuhusiana na tukio la kuuawa kwa wanafunzi wanne, waliodaiwa kuiba komputa na simu za mkononi. Kanda ya video ya kuogofya kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube, ilionyesha wanne hao wakiuawa kinyama. Taarifa zinazohusiana Afrika Wanafunzi wanasema kuwa wanne hao waliuawa baada ya kudhaniwa kuwa wezi kutoka katika kijiji cha Aluu. Chuo kikuu cha Port Harcourt (Uniport) kiliwaamuru wanafunzi kwenda nyumbani,baada ya maandamano yaliyokuwa yanafanyika kukumbwa na ghasia huku Nyumba na maduka zikichomwa. Waandishi wa habari wanasema kuwa polisi wa kupambana na ghasia pamoja na wanajeshi, wameenda katika chuo hicho, ambacho maafisa wakuu wanasema kitasalia kufungwa hadi hali itakapotulia. 13 wakamatwa Wanafunzi waliziba barabara moja kuu karibu na chuo kikuu kwa masaa kadhaa siku ya Jumanne na kuzuia magari kwenda ndani au kutoka nje ya mji wa Port Harcourt. Punde wakaanza kuelekea katika eneo la Aluu, ambako wanafunzi waliuawa na genge la watu mnamo siku ya Ijumaa. Nyumba zilizovamiwa zilikuwa za baadhi ya washukiwa wa mauaji ya wanafunzi hao. Kanda ya video,iliyotumwa katika mtandao wa YouTube mwishoni mwa wiki, inaonyesha wanaume wanne wakivuliwa nguo na kutembezwa uchi kabla ya kuteketezwa. Mmoja wa wanafunzi mwenzao Paul Irabor, aliambia BBC kuwa wanne hao walikuwa wameenda kuchukua pesa walizokuwa wanadai mdeni wao, wakati waliposhambuliwa kwa dhana ya kuwa wezi. Wanafunzi hao inaarifiwa walichukua simu za mkononi na komputa baada ya mdeni wao kukosa kuwalipa ndiposa wakadhaniwa kuwa walikuwa wameiba vitu hivyo. Watu kumi na tatu akiwemo kiongozi mmoja wa kijiji cha Aluu, ambacho kinapakana na chuo kikuu katika eneo linalojulikana kama Choba , wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Thursday, October 4, 2012

Mafuriko Nigeria Yaibua Wanyama Majumbani

*Wanyama hatari kama vile Mamba, Nyoka na Viboko wameanza kuingia kwenye makaazi ya watu katika eneo la kati nchini Nigeria. Mafuriko makubwa yaliyokumba Nigeria yamepelekea mito iliyofurika kusomba wanyama hao hadi kwenye nyumba za wenyeji. "kuna kiboko ndani ya nyumba yangu," Mkaazi wa Jimbo la Benue Wuese Jirake akaiambia BBC. "natarajia kiboko huyo ataondoka atakapochoka kujificha nyumbani kwangu." Mamia ya watu wamefariki na wengine kuachwa bila makao huku mashamba yakiharibiwa na mafuriko hayo makubwa zaidi kuwahi kukumba Nigeria kwa miongo mingi. 'tunatumai yatakwisha' Jirake akaiambia BBC akiongezea kwamba kwa hivi sasa maji yamejaa nyumbani kwake kufikia kina cha kiunoni. "iwapo kuna njia ya kumuondoa kiboko huyu basi maafisa wa Serikali wanafaa kunisaidia." Kulingana na Mwandishi wa BBC Is'haq Khalid, hali kama hiyo pia imeripotiwa katika Miji ya Makurdi, Agatu, Logo na Adoka. Shirika la taifa la kushughulikia hali za dharura limesema linashirikiana na Wakuu wa Jimbo la Benue na wahusika wengine kuhakikisha walioathirika na mafuriko wamerudi kwenye nyumba zao. Mshirikishi wa Shirika hilo katika eneo la kaskazini ya kati nchini Nigeria, Abdussalam Muhammad, ameiambia BBC kwamba sio salama kwa wenyeji kurudi majumbani mwao baada ya wanyama hatari kuingia humo. "kwa hivi sasa kuna Mamba, Nyoka na wanyama wengine hatari waliosombwa na mafuriko kwenye nyumba hizo, na huenda wakawadhuru watu na kuhatarisha maisha yao," akasema. Muhammad amewataka wakaazi kusubiri maagizo kutoka kwa Shirika hilo pale mafuriko yatakapopungua*.(*more info at BBC swahili.com*)