clock
,,,,,
Tuesday, September 25, 2012
Aliyeongeza makalio aamua kuwapa somo wengine madhara yake
MWANAMKE aliyetumia zaidi ya dola 15,000 za Marekani (Sh22.5 milioni) kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa makalio yake, sasa ameandika kitabu kuhusu kile alichokiita siri ya wanawake weusi kuchomwa sindano zenye sumu ili kuongeza ukubwa wa makalio yao.
Vanity Wonder (30), raia wa Marekani ambaye ni mama wa watoto wawili, ameweka bayana kuhusiana na soko la vipodozi feki lililosheheni nchini humo na kuzidi kuingia katika Bara la Afrika ambalo limesababisha yeye kuathirika kutokana na sindano za kemikali ya Siliconi alizochomwa.
"Ndani ya Kitabu changu cha ‘Shot Girls’, nimeelezea kuhusu ufahamu na uzoefu wangu katika shughuli hii ya kuongeza ukubwa wa makalio na jinsi gani nilivyochomwa sindano hizo na jinsi nilivyoweza kuwa msaidizi wa soko la vipodozi hivyo," alisema.
Vanity anaelezea zaidi kuhusiana na mama aliyempeleka binti yake wa miaka 17 na kuweza kumchoma sindano ya kuongeza makalio pamoja na kutengeneza meno feki.
"Manesi na wauguzi, polisi na waimbaji wa nyimbo za injili ni mojawapo kati ya wateja wetu wakubwa na walio wengi ni watu wale ambao wanajua fika kwamba kitendo hiki ni hatarishi," anasema. Vanity anaweka bayana sababu kubwa ya kumfanya aandike kitabu hicho ni kwa kuwa alitaka kuelezea hadithi yake yeye mwenyewe na kuwafafanulia wengi kuhusu imani potofu juu ya siri hii.
Anasema mwaka 2006 ndipo alipoanza kuitafuta sehemu wanakochoma sindano za kukuza makalio na kufanikiwa kuipata, alipewa matibabu aliyoyataka lakini baadaye walimtaka awe mmoja wa watumishi wao.
Anasema alikubali na kuanza kufanya nao.
“Tulikuwa tunanunua kemikali ya ‘silicon’ katika vituo vya gesi," anasema.
Anasema watu wengi huwaeleza wenzao uongo juu ya hilo, hivyo yeye aliamua kuwaacha watu wajaribu na kujionea wenyewe.
“Ni kama kitu cha siri, najitahidi kuwaeleza watu kwa sasa kuliko kuwaacha wajaribu kama nilivyowaacha hapo awali.”
Alisema wanawake kuamua kujibadilisha maumbile yao ni kinyume cha sheria, tamaduni za makabila yote.
Aliongeza kuwa kufanya hivyo pia kunawaweka wanawake katika hatari ya kupata maambukizi ya bakteria au hata kusababisha kifo.
"Si kitu watu wanachofikiri,wapo baadhi ya wasichana ambao wanafanya hivyo kwa kuwa wamemwona mwenzao anafanya," anasema.
Hivi sasa Vanity ambaye ni mama wa watoto wawili anasema si kwamba yeye ameridhika kuwa hivyo, bali ni kati ya wachache ambao hawajapata madhara makubwa kwa sasa na kwamba baada ya miaka kadhaa, anategemea atapata madhara makubwa hivyo anawaonya wale ambao hawajatumia wasiingie katika genge hilo.
Mmoja wa madaktari wanaomtibu, Dk John Martin anasema sindano hizo hutumika kuongeza makalio, mashavu, hips na kwamba ni ghali sana.
"Wakati mwingine hutumia madawa ya viwandani ambayo pia yanaweza kuwa sumu ikiwa mtumiaji atatumia kwa kiasi kikubwa na hivyo unaweza kuishia katika maisha ya taabu na wapo wengine ambao walikatwa sehemu ya viungo vyao na wengine kufa," anasema Dr Martin.(mwananchi.co.tz)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment